Seneta wa Marekani Bernie Sanders ameunga mkono uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kutoa hati za kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na aliyekuwa Waziri wa Ulinzi Yoav Gallant.
Sanders amesema mashtaka hayo yana msingi madhubuti na amesisitiza umuhimu wa Mikataba ya Geneva, inayolenga kulinda raia na kuzuia ukatili wakati wa vita. Huku akikiri haki ya Israel kujilinda, alikosoa idadi kubwa ya vifo vya raia wa Palestina huko Gaza, ambako zaidi ya watu 44,000 wamepoteza maisha, wakiwemo wanawake na watoto.
Kwa mujibu wa Sanders, mashtaka ya ICC dhidi ya Netanyahu na Gallant kwa makosa kama kutumia njaa kama silaha na kushambulia raia yanastahili. Alionya kuwa kutoheshimu sheria za kimataifa kutasababisha kuongezeka kwa ukatili duniani.
Katika hatua ya kihistoria, ICC imetangaza kuwa imepata ushahidi wa kutosha kuhusisha viongozi hao wawili wa Israel na makosa ya kivita katika ardhi za Palestina, ikiwemo Gaza. Mashtaka hayo yanajumuisha “uhalifu wa kivita wa kutumia njaa kama mbinu ya vita, mauaji, mateso, na vitendo vingine visivyo vya kibinadamu.”
Hati hizo za kukamatwa zimetolewa wakati operesheni ya kijeshi ya Israel huko Gaza ikiingia mwaka wake wa pili, huku mahakama hiyo ikisisitiza umuhimu wa kuwajibisha wahusika kwa makosa ya kivita.