Watu wanne wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka manne ikiwemo kutumia jina la Mke wa Rais John Magufuli, Janeth Magufuli kwa ajili ya utapeli wa Mil.4.5
Watuhumiwa hao ni Saada Uledi, Maftah Shaban, Heshima Ally na Shamba Baila ambapo wamesomewa mashitaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Maira Kasonde.
Wakisomewa mashitaka yao na Wakili wa Serikali Batilda Mushi alidai washitakiwa wametenda makosa yao katika nyakati tofauti.
Katika kosa la kula njama ya kutenda kosa inadaiqa kati ya Januari 2017 na Machi 2019 katika maeneo tofauti ya jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine walikula njama ya kutenda kosa la kuchapisha taarifa kupitia mtandao wa Facebook.
Pia katika kosa jingine la kuchapisha taarifa za uongo wanadaiwa katika tarehe hizo ndani ya mkoa wa Dar es Salaam walichapisha taarifa kupitia akaunti ya mtandao wa Facebook ukiwa na jina la Janeth Magufuli ambaye ni mke wa Rais wa Tanzania wakionyesha wana taasisi inayotoa mikopo ambapo wote wanaotaka kupatiwa kuna kiasi cha pesa wanatakiwa kutoa wakati wakijua ni uongo.
Katika kosa jingine ni utakatishaji fedha ambapo wanadaiwa kati ya Machi 2 na 8, 2019 ndani ya Dar es Salaam na mikoa mingine walijipatia kiasi cha Mil.4.5 wakati wakijua ni zao la fedha haramu. Washitakiwa hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi, wamerudishwa rumande, upelelezi wa kesi haujakamilika kesi imeahirishwa hadi Mei 2, 2019.