Wakati ulimwengu ukikabiliwa na changamoto ya kukabiliana na janga la ugonjwa wa Ebola, nchi ya Liberia ambayo imeathiriwa zaidi na ugonjwa huo imetangaza kukabiliwa na upungufu wa mifuko maalum ya kubebea miili ya marehemu waliofariki kwa Ebola.
Serikali ya Liberia imesema kwa sasa ina takribani mifuko 4,900 tu, ikilinganishwa na idadi ya zaidi ya mifuko 85,000 inayohitajika ndani ya kipindi cha miezi sita ijayo.
Takwimu zinaonesha uhaba mkubwa wa vifaa muhimu katika kukabiliana na ugonjwa huo, ikiwa ni pamoja na suti za kujikinga, kifaa maalum cha kujikinga uso, glavu, miwani pamoja na mifuko ya kubebea maiti.
Imeripotiwa kuwa Liberia itahitaji boksi milioni 2.4 ndani ya kipindi cha miezi sita, huku kiasi kilichopo kwa sasa ni boksi 18,000, na kwa upande wa idadi ya kofia zinazohitajika ni milioni 1.2 na kwa sasa inaripotiwa kuwa ziko 165,000. Uhaba huo unatajwa kama kikwazo kikubwa katika kukabiliana na ugonjwa huo ambapo katikati ya wiki hii kuliripotiwa mgomo wa wauguzi wakidai nyongeza ya mshahara.
Tangu kuzuka kwa ugonjwa wa Ebola mwezi wa tatu mwaka huu, takribani watu 9000 wameripotiwa kuathirika, na wengine zaidi ya 4,000 wameripotiwa kupoteza maisha katika nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone kwa mujibu wa takwimu za shirika la afya duniani, huku zaidi ya nusu ya vifo hivyo vikiripotiwa kutokea nchini Liberia.
Taarifa ya shirika la afya duniani (WHO) imetahadharisha kuwa huenda hali ikawa mbaya zaidi siku za usoni katika mataifa hayo matatu na kupelekea idadi ya waathirika kuongezeka na kufikia 10,000 kwa wiki hadi itakapofikia mwisho wa mwaka.
Liberia inatarajia kupokea vifaa mbalimbali wiki ijayo ikiwemo mifuko ya kubebea maiti, lakini taarifa ya shirika hilo inaongeza kuwa vifaa hivyo bado havitoshelezi kukidhi hali ya uhitaji iliyopo katika nchi hiyo.
Mbali ya nchi hizo tatu zinazotajwa kuathiriwa zaidi na ugonjwa wa Ebola, nchi nyingine zilizotajwa kuripotiwa kukumbwa na janga la ugonjwa huo ni pamoja na Senegal, Nigeria, Hispania na Marekani.