Umoja wa ulaya unasema utawawajibisha wanajeshi nchini Niger kwa mashambulio yote dhidi ya raia, wanadiplomasia na balozi baada ya wafuasi wa mapinduzi ya kijeshi kukusanyika nje ya ubalozi wa Ufaransa, na kuteketeza mlango.
Umoja wa Ulaya pia utatumia uamuzi wa viongozi wa Afrika Magharibi wa kuiwekea Niger vikwazo vya kiuchumi kufuatia mapinduzi ya kijeshi, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell alisema katika taarifa yake.
Siku ya Jumapili, maelfu ya watu wanaounga mkono mapinduzi ya kijeshi waliandamana katika mji wa Niamey wakilaani Ufaransa, koloni ya zamani wa nchi hiyo, na kupeperusha bendera za Urusi.
Waandamanaji walichoma moto mlango katika ubalozi wa Ufaransa kabla ya jeshi kuusambaratisha umati huo.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema mashambulio dhidi ya Ufaransa na maslahi yake hayatavumiliwa na kwamba yeyote atakayewashambulia raia wa Ufaransa atawajibishwa.
Ufaransa na EU tayari zimesitisha ushirikiano wa kiusalama na misaada ya kifedha kwa Niger, na kutaka kuachiliwa kwa viongozi waliochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia.