Mwendesha mashtaka anayechunguza shambulio kwenye studio ya TV nchini Ecuador wiki jana ameuawa, maafisa wanasema.
César Suárez aliuawa kwa kupigwa risasi katika mji wa bandari wa Guayaquil, mkoa wa Guayas siku ya Jumatano, mwanasheria mkuu alisema.
Haijabainika iwapo kifo cha Bw Suarez kinahusishwa na uchunguzi wake kuhusu shambulio la kituo cha televisheni.
Wakati wa tukio hilo la kushangaza wiki iliyopita, watu waliojifunika nyuso zao walivamia studio ya kituo cha televisheni cha TC wakati wa matangazo ya moja kwa moja na kuwatishia wafanyikazi kwa kwa kuwaelekezea bunduki.
Picha ambazo zilipeperushwa moja kwa moja hewani zilionyesha mwanahabari Jose Luis Calderon akiwasihi watu hao wenye silaha kutowadhuru huku wafanyakazi wa kituo hicho wakilazimika kuketi au kulala kwenye sakafu ya studio.
Mpiga picha mmoja alipigwa risasi mguuni, huku mkono wa mwingine ukivunjwa wakati wa shambulio hilo, naibu mkurugenzi wa habari wa TC alisema.