Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita imemhukumu kwenda jela miaka mitatu Afisa Tabibu wa Kituo cha Afya cha Katoro, Samson Kuzenza kwa makosa ya kuomba na kupokea rushwa ya Shilingi 30,000 kinyume na kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu mkazi Geita, Obadia Bwegoge ambapo amesema mshtakiwa amepatikana na hatia katika makosa yote mawili ya kuomba na kupokea rushwa kinyume na kifungu cha 15 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa na kwamba atatumikia kifungo cha miaka mitatu jela kwa kila kosa.
Hakimu Bwegoge amefafanua kwamba ushahidl uliowasilishwa na upande wa Jamhuri umethibitisha pasi na shaka kwamba Kuzenza akiwa katika kituo cha kazi Desemba 7, 2019 aliomba rushwa ya Sh 30,000 kutoka kwa, Said Msuluzya ili amfanyie usafi mke wake ambaye ni Sheha Hussein aliyepata tatizo la kuharibikiwa mimba.