Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) limesema Ethiopia inaendelea kukabiliwa na mapigano, idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani, na milipuko ya magonjwa.
Katika ripoti yake ya hivi karibuni kuhusu hali ya kibinadamu nchini Ethiopia, UNICEF imesema hali ya kibinadamu nchini humo imekuwa mbaya zaidi kutokana na athari za hali ya hewa.
Ripoti hiyo imesema, mafuriko yaliyotokea hivi karibuni kutokana na mvua za El Nino yamekuwa na athari kubwa kwa makundi yaliyo hatarini, hususan watoto. Mafuriko hayo pia yameathiri zaidi ya watu milioni 1.5 kusini mashariki mwa Ethiopia, na kusababisha watu laki 6 kukosa makazi na vifo vya watu 57 pamoja na mifugo, na kuharibu mashamba pamoja na miundombinu.
Shirika hilo limeendelea kutoa wito wa ufadhili wa kifedha ili kukabiliana na mahitaji ya watoto, vijana, wanawake na wanaume nchini Ethiopia.