Umoja wa Ulaya umekosoa hali mbaya ya rais aliyezuiliwa wa Niger Mohamed Bazoum, ukitaka aachiwe mara moja baada ya kuondolewa madarakani kwa mapinduzi.
Kwa mujibu wa mkuu wa sera za nje katika umoja huo, Josep Borrell, kuna wasiwasi mkubwa kutokana na hali mbaya ambayo rais anazuiliwa.
EU inasema taarifa za hivi punde zinaeleza kuwa Mohamed Bazoum na familia yake, wamenyimwa chakula, umeme na huduma za matibabu kwa siku kadhaa.
Haya yanajiri wakati huu Marekani nayo ikisema kwamba itawaajibisha wanajeshi waliochukua madaraka nchini humo kuhusu usalama wa rais Mohamed Bazoum, familia yake pamoja na maofisa wote wa serikali wanaozuiliwa.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Antony Blinken pia ameeleza nchi yake inaunga mkono juhudi ya Jumuiya ya ECOWAS kurejesha utawala wa kiraia nchini Niger.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka RFI oinasema kuwa Washington imekuwa ikisistiza kufanyika kwa mazunguzmo kuhusu kinachoendelea nchini Niger kabla ya kutumia nguvu za kijeshi.
Aidha viongozi wa jumuiya ya Ecowas waliokutana mjini Abuja, Nigeria, kujadili mapinduzi yaliyofanyika nchini Niger, kwa pamoja wameunga mkono kuwekwa tayari kwa kikosi cha dharura cha ukanda tayari kuivamia nchi hiyo ikiwa njia nyingine za usuluhishi zitashindikana.