Familia za wale waliouawa katika jaribio la kutoroka kutoka gereza kubwa zaidi nchini Congo, Makala Central Prison, zinataka serikali kutoa majibu kuhusiana na tukio hilo, ambalo takriban watu 129, walipoteza maisha, wengine kwa kupigwa risasi na askari, na wengine kufariki kutokana na msongamano wakati wakijaribu kutoroka.
Hali mbaya za magereza nchini Congo zimekuwa zikilalamikiwa, huku makundi ya haki za binadamu yakisema mazingira hayo ni ya kikatili.
Waziri wa Sheria nchini humo, Constant Mutamba, alitaja tukio hilo kama uharibifu uliopangwa na kuahidi kuchukua hatua kali dhidi ya wahusika. Hata hivyo, makundi ya haki za binadamu na viongozi wa upinzani wanataka uchunguzi huru, wakidai serikali ilitumia nguvu kupita kiasi na kuficha idadi kamili ya vifo. Mmoja wa wanaharakati maarufu anadai kuwa zaidi ya watu 200 waliuawa, wengi wao kwa kupigwa risasi.
Aidha Madeleine Mbalaka, mama wa Everixk Nzeu aliyefariki katika tukio hilo, alieleza majonzi yake kwa kumpoteza mwanawe wa miaka 25 aliyekamatwa miezi miwili iliyopita bila kufikishwa mahakamani. Familia yake hawajaruhusiwa kuuona mwili wake na wanataka maelezo ya kina juu ya kilichotokea, wakiomba haki itendeke kwa wapendwa wao. Mbalaka alisema kuwa alimuona mwanawe siku moja kabla ya tukio hilo akiwa mzima kabisa.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Jacquemin Shabani, alisema kuwa watu 24 waliuawa kwa kupigwa risasi na maafisa wa ulinzi, huku wengine 59 wakijeruhiwa na baadhi ya wanawake wakiripotiwa kubakwa. Hata hivyo, haikuwa wazi kama vifo vyote 129 vilikuwa ni vya wafungwa pekee au ni pamoja na walinzi. Serikali bado haijatoa maelezo kamili juu ya msongamano huo wa vifo.
Jumuiya ya Ulaya imeitaka serikali ya Congo kutoa maelezo haraka juu ya tukio hilo ili kubaini ukweli na kuhakikisha haki za binadamu zinaheshimiwa. Viongozi wa upinzani nchini humo wameelezea kusikitishwa kwao na jinsi serikali ilivyoshughulikia suala hilo, wakidai kuwa vifo hivyo havipaswi kupita bila adhabu kwa waliohusika.