FBI inamsaka mtu anayedaiwa kuwa jasusi wa Iran ambaye inaamini anahusika katika njama za kuwaua maafisa wa sasa na wa zamani wa serikali ya Marekani.
Shirika hilo linamtuhumu Majid Farahani, 42, kwa kupanga njama ya kulipiza kisasi mauaji ya jenerali wa Iran Qasem Soleimani.
Soleimani, kamanda wa kikosi cha Quds cha Iran, aliuawa katika shambulio la ndege isiyo na rubani ya Marekani nchini Iraq mnamo Januari 2020.
FBI inasema Bw Farahani amechukua hatua kwa niaba ya Wizara ya Ujasusi ya Iran.
Katika notisi iliyotumwa Ijumaa, FBI ilisema inamtaka Majid Dastjani Farahani kuhojiwa kuhusiana na kuajiri watu binafsi kwa ajili ya operesheni nchini Marekani.
Maafisa wanasema Bw Farahani husafiri kati ya Iran na Venezuela na pia amewaajiri washirika kwa “shughuli za uchunguzi zinazolenga maeneo ya kidini, biashara na vituo vingine” nchini Marekani.
Mnamo Desemba 2023, Bw Farahani na afisa mwingine anayedaiwa kuwa wa ujasusi waliwekewa vikwazo na hazina ya Marekani.