Katika kupata uelewa wa pamoja kuhusu shughuli za ukaguzi mipakani, Bodi na Menejimenti ya Tume ya Ushindani (FCC) imetembelea Kituo cha ukaguzi wa pamoja (OSBP) kilichopo Sirari Wilayani Tarime Mkoani Mara.
Akizungumza katika ziara hiyo iliyofanyika Jumatatu Julai Mosi, 2024, Bw. William Erio, Mkurugenzi Mkuu wa FCC ambaye pia ndiye Mkaguzi Mkuu wa Alama za Bidhaa Nchini, amebainisha kuwa lengo la ziara hiyo katika Kituo hicho ni kufahamu umuhinu wa kuanzisha ofisi yake katika eneo hilo na kuongeza jitihada za kutokomeza uingizaji wa bidhaa bandia nchini.
Kwa mujibu wa Erio, uanzishwaji wa Ofisi ya FCC katika kituo hicho utaongeza ufanisi katika ukaguzi na udhibiti wa uingizaji wa bidhaa bandia na kuongeza Ushindani katika soko la bidhaa nchini.
“Njia zisizo rasmi katika uingizaji wa bidhaa katika mipaka ya nchi yetu ni tatizo kubwa sana katika Ushindani wa biashara nchini. Nchi yetu ni kubwa na mipaka ni mikubwa kwahiyo inatakiwa kutoa elimu ya kutosha kwa Umma ndio maana tunataka kuanzisha ofisi katika kituo cha pamoja cha ukaguzi,” alisema Erio.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa FCC Dkt. Aggrey Mlimuka, baada ya mazungumzo na wasimamizi wa vitengo mbalimbali vya Serikali ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wamekiri kuhitaji msaada wa FCC katika kuimarisha uingizaji wa bidhaa kutoka nchi jirani.
“Hakuna sababu wala siyo suala la kujadiliana, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alishatoa maelekezo kuhusiana na suala hilo, hivyo Menejimenti tunaenda kujipanga ili tulete watu wa FCC katika kituo hiki kwa ajili ya kuanza kazi. Tupo hapa kuwatumikia watanzania, Serikali ipate mapato na watu wapate bidhaa ambazo zinastahili kuuzwa kwao,” alisema Dkt. Mlimuka.
Akizungumza kwa niaba ya Taasisi za Serikali zilizopo katika kituo hicho, Meneja Msaidizi wa Forodha wa TRA Mkoa wa Mara, Said Hemed, aliahidi kutoa nafasi katika kituo hicho ili kuwezesha uanzishwaji wa Ofisi ya FCC huku akisema uanzishwaji wa ofisi hiyo utaongeza tija kwenye ukusanyaji wa mapato na udhibiti wa uingiaji wa bidhaa zisizo halali.
“Bidhaa mbalimbali za viwandani na zisizo za viwandani zinapitishwa katika mpaka wa Sirari sasa kuna wakati tunashindwa kubaini uhalali wa bidhaa hizo kuingizwa nchini lakini FCC mkianzisha ofisi katika kituo chetu tunaamini itatusaidia kuongeza ufanisi katika maeneo ya ukaguzi na udhibiti,” alisema Hemed.
Ziara ya Bodi na Menejimenti hiyo ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuitaka FCC kuhakikisha inadhibiti uingizaji holela wa bidhaa na udhibiti wa ushindani katika soko la bidhaa nchini.