Shirika la Foundation for Civil Society (FCS) na Vodacom Tanzania Foundation wamesaini makubaliano ya mkataba wa mwaka mmoja wenye thamani ya shilingi milioni 150, kwa lengo la kudhamini Wiki ya AZAKi 2024 itakayofanyika Jijini Arusha kuanzia Tarehe 9 hadi 13 Septemba, 2024.
Akizungumza katika hafla fupi ya kusaini makubaliano hayo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa FCS, Justice Rutenge, amesema kiasi hicho cha fedha kutoka Vodacom Tanzania Foundation, ambayo ni mdhamini mkuu wa wiki hiyo, kimeongeza chachu ya ushirikiano wa pamoja katika kukuza maendeleo ya jamii kupitia Wiki ya AZAKi.
Rutenge ameeleza kuwa ili tuweze kusonga mbele kuifikia Tanzania tunayoitaka, sauti za wadau na wabia mbalimbali zinahitajika kusikika na ziwe sehemu ya kutoa mchango katika mchakato mzima wa maendeleo ambayo yatasaidia kujenga maono ya kulipeleka Taifa letu mbele.
Katika kufanikisha Wiki ya AZAKi, FCS wamechangia shilingi milioni 250, ambapo michango mingine inatoka kwa wadau wa maendeleo zikiwemo asasi za kiraia.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Foundation Tanzania, Zuweina Farah, amesema ili kufanikisha dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, ushirikiano wa pamoja unahitajika kati ya AZAKi, sekta binafsi na Serikali.
Pia ameongeza kuwa, lengo la Vodacom Foundation Tanzania ni kukuza ushirikiano katika kuleta maendeleo ya jamii, kuimarisha utawala bora, kuboresha mazingira ya biashara na kusaidia jamii kupitia elimu afya na teknolojia
Wiki ya AZAKi mwaka huu imebebwa na kauli mbiu ya Sauti, maono na thamani ambayo inachagiza kauli mbiu ya FCS ya kuwezesha ushirikiano kwa maendeleo.