Leo February 4, 2018 Polisi wanadaiwa kumteka nyara Padri Sebastian wa kanisa Katoliki baada ya ibada kumalizika ikiwa ni kwa mujibu wa taarifa za mashuhuda waliokuwa nje ya Kanisa katika Mji mkuu wa Kinshasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.
Hayo yanatokea wakati mivutano kati ya kanisa Katoliki na serikali ya DRC ikizidi kushika kasi kufuatia hatua ya Rais Joseph Kabila kukataa kuondoka madarakani baada ya muda wake kwa mujibu wa katiba kumalizika.
Shuhuda mmoja katika kijiji cha N`sele mashariki mwa mji wa Kinshasa amelieleza shirika la habari la AFP kuwa polisi walimkamata Padri Sebastian Yebo baada ya Ibada ya asubuhi na kumpakiza kwenye gari aina Jeep na kuondoka naye.
Hata hivyo Polisi walikataa kuzungumzia tukio hilo walipoulizwa na shirika la habari la AFP. Tukio hilo linakuja ikiwa ni baada ya operesheni iliyofanywa na serikali dhidi ya waratibu wa maandamano ya waumini wa kanisa Katoliki kupinga rais Kabila kuendelea kubakia madarakani.
“HUU NI UHUJUMU UCHUMI, WOTE TUTAWACHUKULIA HATUA” -NAIBU WAZIRI MWANJELWA