Serikali imewahakikishia Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, kuwa inayachukulia kwa uzito mkubwa, maoni na mapendekezo yao kuhusu maboresho ya Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako, amesema hayo wakati akifunga Kikao Kazi cha Mafunzo ya Uelimishaji kwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Kanda ya Kusini na Watendaji wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) Mjini Songea leo February 10, 2024.
Profesa Ndalichako amesema tayari inayafanyia kazi baadhi ya mapendekezo ya maboresho ya sheria yaliyotolewa na Majaji kwenye kikao kazi kama hicho kilichofanyika Mjini Bagamoyo mwezi July, 2023
“Mapendekezo ya kuboresha kifungu cha 39 (2) cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi [Sura 263] kilichoweka ukomo wa muda wa kuwasilisha madai bila kutoa wigo wa kupokea madai hayo iwapo kuna sababu za msingi za kucheleweshwa, tumeyafanyia kazi na tunataraji muswada wa marekebisho kuwasilishwa Bungeni hivi karibuni.”
Profesa Ndalichako amesema Ofisi yake kupitia Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi inatarajia kupokea maoni zaidi kutoka kwa Majaji kwa lengo la kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi [Sura 263].
“Natamani kuona kuwa kati ya mapendekezo yenu katika mafunzo haya iwe ni namna gani rahisi tunaweza kutumia sheria kuwezesha Waajiri wote ambao hawajajisajili WCF, kufanya hivyo mara moja,”
Ndalichako pia amesema Serikali ya awamu ya Sita chini ya Uongozi mahiri wa Rais Daktari Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua na kuthamini mchango wa Wafanyakazi katika Sekta zote na ndio maana imeendelea kutekeleza na kuboresha masuala ya fidia kwa wafanyakazi katika sekta binafsi na umma
Amesema, katika kipindi kifupi cha Uongozi wa Serikali ya awamu ya sita kumeshuhudiwa mabadiliko mbalimbali katika Sekta ya Hifadhi ya Jamii ikiwemo kupunguza kiwango cha uchangiaji kwa Waajiri wa Sekta binafsi kutoka asilimia 1 ya mshahara wa mfanyakazi kila mwezi hadi kufikia asilimia 0.5.