FIFA imetangaza matumizi ya ishara mpya ya mikono, inayojulikana kama CROSSED HANDS, kama hatua ya kupambana na ubaguzi wa rangi kwenye mechi za kandanda.
Taarifa hiyo ilitolewa baada ya kupitishwa kwa ishara hiyo kwa kauli moja katika Kongamano la 74 la FIFA lililofanyika Bangkok, Thailand mnamo Mei 17, 2024. Ishara hii itaanza kutumika rasmi katika Kombe la Dunia la Wanawake wa Umri wa Miaka 20 litakalofanyika nchini Colombia mwaka 2024.
Kwa kutumia ishara hii, wachezaji wataweza kukunja mikono yao kwenye ili kuashiria mwamuzi endapo wanakabiliwa na ubaguzi wa rangi.
Hatua ya kwanza itakuwa kuacha mchezo kwa muda, hatua ya pili itakuwa kusimamisha mchezo ikiwa ubaguzi utaendelea, na hatua ya tatu ni kuacha mchezo kabisa ikiwa tatizo halitaisha.
Rais wa FIFA, Gianni Infantino, alisema kuwa utumiaji wa ishara hii ni hatua muhimu katika kuimarisha uwezo wa wachezaji duniani kote na kuonyesha dhamira ya FIFA katika kupambana na ubaguzi wa rangi.
Infantino aliongeza kuwa wanachama wote 211 wa FIFA walikubaliana kwa kauli moja na hatua hii katika Kongamano la FIFA, na kuahidi kwamba FIFA itafanya kazi na serikali na mamlaka za polisi ili kuhakikisha kwamba wale wanaoshughulika na ubaguzi wanashughulikiwa.
Kabla ya hili, FIFA ilizindua kampeni ya Hapana kwa Ubaguzi katika Kombe la Dunia la 2022 lililofanyika Qatar, ambayo ililenga kuongeza uelewa, elimu, na kuchukua hatua dhidi ya aina zote za ubaguzi katika mchezo.