Leo June 25, 2018 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeahirisha kesi inayowakabili Viongozi wa CHADEMA akiwemo Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe hadi June 27,2018 kwa sababu Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Vicent Mashinji hakufika mahakamani.
Hatua hiyo imefikiwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri baada wakili wa serikali, Faraja Nchimbi kueleza kuwa kesi hiyo imeitishwa ili washtakiwa wasomewe maelezo ya awali lakini mshtakiwa wa 6, Dk.Vicent Mashinji hayupo mahakamani.
Wakili wa utetezi, Peter Kibatala amedai kuwa Dk. Mashinji ana udhuru yupo katika mahakama ya Songea ana kesi nyingine, hivyo wanaomba ahirisho.
Maombi hayo ya ahirisho yaliibua mvutano wa kisheria baada ya wakili wa serikali Paul Kadushi kutaka kesi iahirishwe hadi kesho, huku wakili Kibatala akitaka iahirishwe hadi tarehe nyingine.
Kutokana na mvutano huo, Hakimu Mashauri ameahirisha kesi hiyo hadi June 27,2018
Mbali ya Mbowe na Mashinji, washtakiwa wengine ni Mbunge wa Iringa Mjini Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu na Naibu katibu Mkuu bara na Mbunge wa kibamba John Mnyika.
Pia mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe Halima Mdee na mbunge wa bunda, Esther Bulaya na mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko.
Kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13 ikiwemo kula njama, ambapo inadaiwa February 1 na 16, 2018, Dar es Salaam walikuĺa njama ya kutenda kosa la kufanya mkusanyiko usio halali na kukiuka tamko kutawanyika.
Wanadaiwa kuwa February 16,2018 katika barabara ya Kawawa Kinondoni Mkwajuni washtakiwa hao wakiwa na wenzao 12 ambao hawapo mahakamani walikiuka tamko la kuwataka kutawanyika la Afisa wa polisi SSP, Gerald Ngiichi kwa kugoma kutawanyika na kupelekea uvunjifu wa amani.
Inadaiwa kugoma huko kulipeĺekea hofu na hatimaye kusababisha kifo cha Akwilina Akwiline na majeruhi kwa askari wawili ambao ni H.7856 PC Fikiri na E.6976 CPL Rahim Msangi.
Mbowe alivyofika mahakamani Kisutu baada ya kufiwa na Kaka yake