Mechi ya 3 ya hatua ya 16 bora ya kombe la dunia imepigwa usiku wa leo kati ya Uholanzi na Mexico.
Mchezo huo uliopigwa huko Forteleza, umeisha kwa timu ya Louis Van Gaal kutinga robo fainali kwa ushindi wa shida wa 2-1 dhidi ya Mexico.
Mexico walikuwa wa kwanza kupata goli dakika 3 baada ya kipindi cha pili kuanza, Giovan Dos Santos akiweka kambani kwa shuti kali.
Wakicheza bila baadhi ya wachezaji wao muhimu, Uholanzi ilijaribu kwa kila hali kusawazisha goli hilo lakini ugumu wa ngome ya Mexico chini ya kipa Ochoa ulikuwa imara.
Zikiwa zimebaki dakika mbili kabla ya mpira kuisha, Wesley Sneijder akaisawazishia Uholanzi, kabla ya dakika kadhaa mbele Arjen Robben akafanyiwa madhambi na Marquez kisha Klaas Jan Hunterlaar kuweka kimiani penati hiyo na hivyo kuipeleka Uholanzi kwenye robo fainali.
Mshindi wa mechi inayoendelea hivi sasa kati ya Costa Rica vs Ugiriki ndio atacheza na Uholanzi wikiendi ijayo.