Hukumu hiyo imetolewa leo Machi 27, 2024 na Mheshimiwa Hakimu Nyella mbele ya mahakama ya hakimu mkazi wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro baada ya kujiridhisha na ushahidi uliotolewa pasi na shaka kwamba mtuhumiwa Damiani Anthony Matias, (28) fundi ujenzi alimbaka mwanafunzi wa darasa la kwanza, mwenye umri wa miaka 7 wa shule ya msingi Redeemed iliyopo wilayani humo.
Damiani alitenda kosa hilo Septemba 27, 2023 huko maeneo ya Tarakea Kibaoni wilaya ya Rombo ambapo alikamatwa na kufikishwa Mahakamani Oktoba 04, 2023 na kesi hiyo kusajiliwa kwa namba CC 160/2023 chini ya Mpelelezi wa Polisi Sajenti Mzigo.
Akisoma hukumu hiyo Mheshimiwa hakimu Nyella amesema amemtia hatiani Mtuhumiwa huyo kwa kosa la ubakaji na kutoa adhabu kali ya kifungo cha maisha jela iwe fundisho kwa wengine wenye tabia za kutenda makosa ya ukatili dhidi ya watoto.
Mheshimiwa Nyella ameacha wazi nafasi ya mtuhumiwa kukata rufaa iwapo hajaridhika na hukumu iliyotolewa.