Muswada wa kutaka kubatilisha marufuku ya Gambia dhidi ya ukeketaji (FGM) uliwasilishwa katika Bunge la nchi hiyo ya Afrika Magharibi jana Jumatatu na unatarajiwa kujadiliwa na wabunge baadaye mwezi huu.
Rais wa zamani wa gambia, Yahya Jammeh, alipiga marufuku tabia hiyo mwaka wa 2015 na kuainisha faini kali na vifungo jela kwa wahalifu watakaokiuka marufuku hiyo.
Hata hivyo, wananchi wengi wa Gambia bado wanaamini kuwa ukeketaji wa wanawakke ni suala ya kidini na kiutamaduni, na muswada huo uliowasilishwa na mbunge Almameh Gibba unasema kuwa, marufuku ya sasa inakiuka haki za raia kutekeleza utamaduni na itikadi zao za kidini.
Muswada huo umegawanya maoni ya umma nchini Gambia. Watetezi wa marufuku ya ukeketaji wanaashiria madhara ya kimwili na kisaikolojia ya mila hiyo kwa wasichana na wanawake wakisema kuondolewa kwa marufuku hiyo itakuwa hatua ya kurudi nyuma.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linasisitiza kuwa, kitendo hicho hakina faida za kiafya na kinaweza kusababisha matatizo mengi kkwa siha za wanawake.
Muswada wa kujadili marufuku ya ukeketaji wa wanawake nchini Gambia unatazamiwa kujadili tena 18 Machi katika Bunge la Gambia.