Israel na Hamas, hatimaye zimeanza kutekeleza makubaliano ya usitishaji mapigano kwa siku 4, makubaliano yatakayoshuhudia kuanza kuwasili kwa misaada ya kibinadamu na kuachiwa kwa kundi la kwanza la mateka wanaoshikiliwa na Hamas kwenye eneo la Gaza.
Baada ya majadiliano ya majuma kadhaa na mwanzoni mwa juma hili kufikia makubaliano, usitishwaji wa mapigano ulianza saa moja kamili asubuhi hii kwa saa za Israel.
Kwa mujibu wa nchi ya Qatar, punde baada ya saa moja kutimia, magari ya misaada ya kibinadamu yalianza kuingia kwenye eneo la Gaza kupitia mpaka wa raffah nchini Israel.
Aidha baadae hivi leo majira ya sakumi jioni saa za Israel ambapo Afrika mashariki itakuwa ni saa kumi na moja, kundi la kwanza la mateka 13 kati ya 50 wataachiwa na kundi la Hamas.
Pamoja na haya, Israel pia inatarajiwa kuwaachia huru zaidi ya wafungwa 150 wa Kipalestina wanaoshikiliwa kwenye magereza yake.