Ukanda wa Gaza uko ukingoni mwa hatari kubwa ya kiafya huku kukiwa na mzingiro unaoendelea, kulingana na kamishna mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA).
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Jerusalem, Philippe Lazzarini alionya siku ya Ijumaa kuwa maji, chakula na dawa vinapungua huko Gaza.
Lazzarini aliendelea kusema kwamba alionya siku chache zilizopita kwamba UNRWA haitaweza kurejea kazi yake ya usaidizi wa kibinadamu ikiwa usambazaji wa mafuta hautaruhusiwa kuingia katika eneo hilo.
Alisema kuwa lori chache za misaada zinazoruhusiwa kuingia Ukanda wa Gaza hazitoshi na usitishaji mapigano unahitaji kuhakikishwa huku kukiwa na kuporomoka kwa jumla kwa sekta ya afya.
Kulingana na afisa huyo, wafanyakazi wasiopungua 57 wa UNRWA wameuawa tangu Oktoba 07.
Lazzarini alisema kuwa UNRWA inafuata mifumo thabiti ya kuhakikisha kuwa misaada haiangukii katika mikono isiyofaa.
Mgogoro huko Gaza ulianza wakati kundi la Palestina Hamas lilipoanzisha Operesheni Al-Aqsa Flood – shambulio la kushtukiza la pande nyingi mnamo Oktoba 7 ambalo lilijumuisha safu ya kurusha roketi na kujipenyeza ndani ya Israeli kwa ardhi, bahari na angani.
Hamas imesema uvamizi huo ulikuwa wa kulipiza kisasi kuvamiwa kwa Msikiti wa Al-Aqsa na kuongezeka kwa ghasia zinazofanywa na walowezi wa Israel dhidi ya Wapalestina.