HABARI YA ASUBUHI NA KARIBU KWENYE MATANGAZO YETU HII LEO…
Shirika la afya duniani, WHO, limesema limefanikiwa kuwahamisha watoto njiti zaidi ya 30 kutoka katika hospitali kubwa zaidi kwenye eneo la Gaza, shirika hilo likisema linapanga kuwandoa wafanyakazi wa hospitali hiyo katika kile imesema eneo la ukanda wa vifo.
Hatua ya WHO imekuja saa chache tangu ujumbe wake utembelee hospitali ya Al Shifa, ambayo juma lililopita ilivamiwa na wanajeshi wa Israel.
Aidha rais wa kamisheni ya umoja wa Ulaya, Ursula von de Leyen, amesema suluhu ya kisiasa ndio njia pekee ya kuleta amani kati ya Israel na Palestina.
‘‘Hata wakati tunapowazia leo lazima pia tufikirie siku zijazo zitakuwa aje na namna raia wa Israeli na Palestina wanaweza kuwa na matumaini tena.’’ alisema Ursula von de Leyen.
Haya yanajiri wakati huu Israel ikitoa picha za CCTV ilizosema zinaonesha mateka wakipelekwa kwenye hospitali hiyo na wapiganaji wa Hamas.
Katika upande mwengine, China imesema iko tayari kusaidia katika urejeshaji wa amani katika eneo la Mashariki ya kati.