Geita Gold Mining Limited (GGML) imepokea ruhusa ya mpango wa uchimbaji madini wa mwaka 2021 unaohusisha uchimbaji wa wazi na wa chini kwa chini.
Mkaguzi Mkuu wa Migodi yote nchini Dkt. Abdul Rahman Mwanga ameruhusu mpango huo baada ya GGML kupeleka nyaraka zote Tume ya Madini na kupatiwa vibali.
Kufuatia ruhusa hiyo, GGML sasa inatarajiwa kufanya shughuli zake za uchimbaji kama zinavyoainishwa kwenye kijitabu kilichokamilika na kutiwa saini na Mkaguzi Mkuu wa migodi yote nchini.
GGML inapaswa pia kuendesha shughuli zake kwa kuzingatia masharti na miongozo ya sheria za nchi ya Tanzania.
Vile vile, Kampuni itaweka taarifa mpya kila mwaka katika mpango wa uchimbaji uliothibitishwa na kwa kuzingatia mabadiliko makubwa katika shughuli za uchimbaji.
Akizungumzia ruhusa hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa GGML Bw. Richard Jordinson ameipongeza serikali kwa kuendeleza ushirikiano wa miaka mingi na kufafanua kuwa GGML sasa itapata fursa ya kupanua wigo zaidi wa uzalishaji na kutimiza matarajio ya wadau wake.
“Kupata kibali cha mpango huu wa uchimbaji ni ushahidi wa rekodi yetu nzuri ya uchimbaji madini nchini. Hii inaonyesha pia imani iliyonayo Serikali kwa kampuni yetu kama mdau wa maendeleo,” Jordinson.
Miradi inayotajwa katika mpango wa uchimbaji wa GGML ni pamoja na Mradi wa Nyamulilima utakaohusisha maeneo ya kituo cha nane (8), Star and Comet, Xanadu, Selous, Mabe pamoja na Roberts.
Uchimbaji wa wazi katika eneo la Nyamulilima unatarajiwa kuongeza uzalishaji dhahabu katika mgodi wa GGML ambapo uchimbaji unaweza kuendelea hadi mwaka 2027.
Ruhusa ya kuanza shughuli za uchimbaji katika eneo la Nyamulilima ni habari njema kwa wadau wetu, wafanyakazi na wakandarasi.
Inatoa pia fursa nyingi kwa jamii inayotuzunguka kufaidika kutokana na shughuli za AngloGold Ashanti. Tunatarajia kuendelea kufanya uwekezaji kwenye jamii inayotuzunguka kwa kuwa hiyo ni mojawapo ya tunu zetu,” aliongeza Bw Jordinson.
Hivi karibuni GGML iliibuka mshindi wa jumla wa kampuni zinazofanya vizuri kwenye sekta ya madini nchini Tanzania kwa mwaka 2019/2020. GGML iliibuka mshindi katika vipengele vya Wajibu wa Kampuni kwa Jamii (CSR), Utunzaji mazingira na usalama, ukusanyaji wa mapato ya Serikali (kodi) pamoja na uwezeshaji wa wazawa.