Katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru, Tanzania imefanikiwa kuchimba visima 96 vya mafuta na gesi ambapo visima 44 vimegundulika kuwa na gesi asilia.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Mhandisi Charles Sangweni wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ikiwa ni mwendelezo wa wizara na tasisi zake kuelezea miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania.
Mhandisi Sangweni alisema kuanzia mwaka 1960 kumekuwepo na juhudi za kutafuta mafuta na gesi asilia ambapo visima 96 vimechimbwa, 59 vikichimbwa nchi kavu na 37 baharini.
Amesema katika visima 44 ambavyo vimegundulika kuwa na gesi asilia visima 16 ni nchi kavu na 28 ni baharini na kwamba juhudi za utafiti zinaendelea ili kupata vyanzi vingine.
Kaimu mkurugenzi huyo alisema hadi sasa wamefanya utafiti kwenye eneo la mraba 534,000 ambapo kilomita za mraba 394,000 ni nchi kavu na kilomita 140,000 ni baharini.
“Tunaadhimisha miata 60 tukiwa tumefanikiwa kuchimba visima 96 ambapo visima 44 vimegundulika kuwa na gesi asilia ambayo nyingine ndio inatumika kuzalisha nishati ya umeme kwa asilimia 60, PURA tunaendelea kuhamasisha wawekezaji katika eneo hilo ili waje kuwekeza na kutafuta vyanzo vingine,” Mhandisi Charles Sangweni
Sangweni alitaja maeneo yenye visima ni pamoja na Ruvu, Mkuranga Pwani, Ntorya, Mnazibay (Kijiji cha Msimbati mkoani Mtwara na SongoSongo mkoani Lindi.
Amesema uzalishaji gesi ulianza mwaka 2004 kwa upande wa SongoSongo na mwaka 2006 kwa upande wa Mnazi Bay ambapo ambapo gesi iliyogunduliwa ni futi za ujazo trilioni 57.54, nchi kavu ikiwa futi za ujazo trilioni 10.06, baharini trilioni 47.48.
Mhandisi Sangweni alisema uamuzi wa Serikali kuanzisha PURA mwaka 2015 umeongeza kasi ya utafutaji wa mafuta na gesi na kuwataka wadau wote kwenye sekta hiyo kuwekeza katika eneo hilo muhimu kwa uchumi wa nchi.
Amesema hadi sasa Tanzania ina mikataba ya Utafutaji, Uendelezaji na Uzalishaji Mafuta na Gesi Asilia (PSA) 11, kati ya hiyo mitatu ipo katika hatua za uzalishaji na nane katika hatua mbalimbali.
Sangweni amesema pia kwa miaka ya hivi karibuni sekta hiyo imefanikiwa kushirikisha Watanzania kwa asilimia 90 kwenye kampuni zenye PSA.
“Ila jambo zuri zaidi kumeimarika kwa shughuli za ukaguzi wa gharama za matumizi katika mikataba ya PSA, ambapo hadi sasa tunatimiza miaka 60 kaguzi hizi zimewezesha kuokoa zaidi ya Sh bilioni 90,” Mhandisi Charles Sangweni
Alisema wamepitia changamoto mbalimbali lakini kwa kushirikiana na Serikali zimekuwa zikitatuliwa ambapo kwa sasa Tanzania inazalisha gesi asilia nyingi na mikakati yao ni kuongeza uzalishaji zaidi ili kushikiri kikamilifu kuifikisha nchi uchumi wa viwanda kufikia 2025.
Mhandisi Sangweni alisema mafanikio zaidi yatapatikana kupitia Mradi wa Usindikaji Gesi kuwa Kimiminika (LGN), ambapo fedha, ajira na viwanda vinavyotumia gesi kama malighafi vitaongeza uzalishaji.