ZAIDI ya madereva bodaboda 200 wa jiji la Arusha wamepatiwa mafunzo maalum ya usalama na afya kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kutambua vihatarishi vya ajali na magonjwa katika shughuli zao za uzalishaji.
Mafunzo hayo yaliyotolewa na Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa ushirikiano na Wakala wa Afya na Usalama Mahali pa Kazi (OSHA), ni sehemu ya programu za kutoa elimu ya usalama na afya miongoni mwa makundi mbalimbali ya wajasiriamali wadogo ambayo imetolewa katika wiki ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa usalama na afya mahali pa kazi.
Akitoa mafunzo hayo kwa madereva hao, Meneja Mwandamizi wa Afya, Usalama na Mazingira kutoka GGML, Dk Kiva Mvungi aliwasihi madereva hao kujiepusha na ajali zinazozuilika kwa kuheshimu alama pamoja na barabarani.
Aidha, alitoa wito kwa madereva hao kujenga tabia ya kupima afya mara kwa mara ikiwamo magonjwa yasiyoambukiza kama vile kisukari, presha na moyo ili kufanya kazi hiyo kwa utulivu.
“Lakini sio kila namba unayopewa na mdada unaisave, watawachukulia hela zenu zote. Jifunzeni kuhifadhi fedha ili baada ya muda uwe na bodaboda yako binafsi au uongeze nyingine na hata kufungua biashara mbalimbali,” alisema.
Naye Ofisa usimamizi wa afya na usalama mahali pa kazi kutoka GGML, Kulwa Simba alisema mafunzo hayo yalilenga kuwasaidia madereva hao namna ya kutambua na kujikinga ili kutoingia kwenye ajali zisizo za lazima.
“Pia tumewafundisha namna ya kuokoa mtu aliyepata ajali ya bodaboda kwa sababu ilikuwa ni utamaduni kwamba ajali ni sehemu ya maisha yao. Lakini tumewasisitiza kwamba dereva mmoja ana familia, ndugu na jamaa wanaomtegema hivyo ni vema kuwa makini.
Aidha, Kulwa aliongeza kuwa GGML iliwagawia washiriki hao baadhi ya vifaa kinga yakiwemo mavazi yanayomtambulisha mtu akiwa katika eneo la kazi (reflective vests) 300.
Awali akifunga mafunzo hayo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Deogratius Ndejembi aliwapongeza washiriki kwa kutambua umuhimu wa mafunzo hayo na kujitokeza kwa wingi ambapo amewataka kutumia ipasavyo maarifa waliyoyapata katika kuboresha kazi yao ya usafirishaji.
“Baada ya mafunzo haya sitarajii kuona mtu yoyote miongoni mwenu anakuwa sehemu ya waendesha pikipiki wanaovunja sheria za barabarani ikiwemo kuvipita vyombo vingine vya moto bila kuwa na tahadhari yoyote. Niwahakikishie kuwa Serikali yenu chini ya Rais wetu Samia Suluhu Hassan, inawathamini na itaendelea kuwapa mafunzo pamoja na fursa za mitaji ili muweze kujiinua kiuchumi,” alisema.
Akimkaribisha Waziri kufunga mafunzo hayo, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, aliwapongeza washiriki wa mafunzo kwa kujitoa na kutenga muda wao ambao wangeutumia kufanya shughuli zao za uzalishaji.
Akitoa shukrani kwa niaba ya washiriki wenzake, Mwenyekiti wa Umoja wa Boda Boda Wilaya ya Arusha, Okelo Costantine, aliishukuru serikali kwa kuendelea kuwapigania vijana kufanya kazi zao kwa utulivu pamoja na kuwapatia fursa mbali mbali zikiwemo za mafunzo.
Mafunzo hayo ambayo yamefanyika tarehe 29 Aprili 2024 katika Uwanja wa General Tyre uliopo Njiro Jijini Arusha, yalijumuisha mada mbalimbali zikiwemo utambuzi wa vihatarishi vya usalama na afya katika shughuli za usafirishaji pamoja na utoaji wa huduma ya kwanza kwa waathirika wa matukio ya ajali za barabarani.