Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imeahidi kuendelea kushirikiana na Serikali kupitia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) katika kuendeleza tafiti na ubunifu zinazoendelea kufanyika ndani ya nchi ili kutoa majibu ya changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii ya watanzania.
Hayo yamebainishwa mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam na Makamu Rais wa AngloGold Ashanti – GGML anayeshughulikia miradi endelevu na masuala ya ubia na ushirika Afrika, Simon Shayo wakati akizungumza katika hafla ya kuhitimisha maadhimisho ya 9 ya Wiki ya Utafiti na Ubunifu Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM).
GGML ilikuwa mmoja wa wadhamini wakuu wa wiki hiyo ya utafiti na ubunifu ambayo imeshuhudia miradi 306 ikioneshwa.
Mbali na kuipongeza UDSM kufanya juma lililopita kuwa la utafiti na ubunifu, pia alihidi kuwa GGML itaendelea kuwa wadhamini wa wiki hiyo ili kuchochea miradi zaidi ya kiutafiti na kiubunifu nchini.
“Tunaona tuendelee kuwa wabia katika hili kwasababu tunaamini kwamba hakuna nchi duniani iliyopiga hatua kubwa kimaendeleo bila kujikita kwenye utafiti na ubunifu. Nchi tulizokuwa nazo miaka 20 au 25 iliyopita kama Malaysia, Singapore na nyingine wamewekeza zaidi kwenye utafiti na ubunifu ndio maana tunaona hatua walizopiga.
“Hivyo sisi kampuni ya madini tunaamini kwamba uwepo wetu hapa nchini kwa miaka 25, tumekuwa sehemu ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2025 na tunaamini tutakuwa sehemu ya Dira ya Taifa ya 2050 ndio maana tunapenda kuwaambia kwamba tutaendelea kushirikiana nanyi na tutaendelea kuwa wadhamini wa tuzo hizi kwenye maeneo ya watafiti,” alisema.
Aidha, alitoa changamoto hasa kwa wanafunzi kutumia fursa hizo za utafiti pamoja na kujifunza hasa ikizingatiwa matokeo ya bunifu hizo huwa zinatumiwa katika maeneo mbalimbali ikiwamo kwenye sekta ya madini.
Alisema katika kuendeleza vipaji vya wahitimu pamoja na kuwaongezea uzoefu kwenye taalumazao, GGML kila mwaka huchukua wahitimu 60 kutoka vyuo mbalimbali nchini na kuwapatia mafunzo hayo kwa mwaka mmoja.
Alisema wahitimu hao ambao asilimia 50 huwa ni wanawake, hupewa uzoefu katika maeneo mbalimbali ya sekta ya uchimbaji ikiwamo utafiti wa kijiolojia.
Awali akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Franklin Rwezimula mbali na kuipongeza GGML kwa kudhamini maadhimisho hayo, pia alitoa wito kwa kupanua wigo wa wiki ya utafiti na ubunifu kwa kushirikisha washirika wa utafiti ambao tafiti zao zimesajiliwa na zina uhusiano na idara mbalimbali za kitaaluma.
“Matokeo ya tafiti zinazofanywa na vyuo mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yamekuwa ni rejea muhimu katika utekelezaji wa sera, mipango na mikakati mbalimbali ya kitaifa, kikanda na kimataifa katika masuala ya utafiti na ubunifu.
“Maadhimisho haya yanatoa jukwaa zuri la kuhamasisha kizazi cha wanataaluma wachanga na chipukizi kufanya utafiti na ubunifu unaojibu changamoto za kiuchumi na kijamii katika nchi yetu na dunia kwa ujumla,” alisema
Alisema ikiwa vyuo vikuu nchini Tanzania vitaonesha kwa umma kazi zao za kitaaluma na zinazotokana na matokeo ya utafiti, vitaishawishi serikali na soko la ajira, kuboresha uhusiano uliopo baina ya vyuo vikuu na waajiri na wafadhili na hatimaye kutoa fursa ya ushirikiano ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake Kaimu Naibu Makamu Mkuu Wa Chuo – Utafiti, Prof. Nelson Boniface aliishukuru GGML kwa kufanikisha maadhimisho hayo ambayo yalihusisha wafanyakazi na wanafunzi kushiriki kuonesha shughuli na miradi yao mbalimbali ya utafiti na ubunifu katika ngazi husika.
“Katika ngazi ya Vitengo, jumla ya miradi 306 ilionyeshwa ambayo ilikuwa katika maeneo (categories) makundi tisa (9). Kati ya kazi hizo, kazi 205 (67%) zilionyeshwa na wafanyakazi na wanafunzi wanaume huku kazi 101 (33%) zilionyeshwa na wafanyakazi na wanafunzi wanawake.
“Kati ya kazi 306 za mwaka huu, kazi za wafanyakazi zilikuwa 82 (27%) na za wanafunzi zilikuwa 224 (77%). “Hii inaonesha ni kiasi gani Chuo chetu kimejikita katika kuhamasisha wanafunzi wetu kuwa sehemu ya watafiti na wabunifu na kuwajengea uwezo kuwa chachu ya maendeleo ya nchi yetu,” amesema.
Maadhimisho hayo yalibeba ujumbe usemao ”Kukuza utafiti na ubunifu kupitia ubia baina ya chuo kikuu cha Dar es Salaam na Tasnia mbalimbali.