JITIHADA za Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) katika kuzingatia uwajibikaji wake kwa jamii pamoja na kuzingatia masuala ya usalama kazini, zimeendelea kuthibitika baada ya kampuni kujinyakulia tuzo mbili katika Kongamano la Kimataifa la Madini na Uwekezaji Tanzania 2023.
Kongamano hilo lililozinduliwa na Naibu Waziri Mkuu. Dk. Doto Biteko jana mchana, lilifuatiwa na hafla ya Usiku wa Madini ambayo pamoja na mambo mengine ilishuhudiwa GGML ikibeba tuzo ya mshindi wa jumla katika kundi la Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR).
GGML pia ilinyakua tuzo ya kuwa kampuni bora inayozingatia masuala ya uhifadhi mazingira na uzingatiaji wa masuala ya afya na usalama mahala pa kazi.
Tuzo hizo zilizotolewa na wizara ya madini katika kuchagiza kongamano hilo, zimeifanya GGML kuiendelea kuwa kampuni inayoongoza nchini kwa kuzingatia masuala ya afya na usalama mahala pa kazi kwani katika kipindi cha miaka minne mfululizo imebeba tuzo hizo zinazotolewa na Kampuni mama ya AngloGold Ashanti yenye migodi katika nchi mbalimbali duniani.
Akizungumza katika hafla hiyo ambayo pia ilihudhuriwa na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde na viongozi wa Serikali kutoka Uganda, Malawi na nchi nyingine, Waziri wa Madini wa Malawi, Monica Chang’anamuno aliipongeza GGML kwa kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali ya Tanzania katika kuwainua wananchi wake kiuchumi.
Waziri huyo ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, pia aliipongeza GGML kwa kufanikisha kongamano hilo ambalo limeshirikisha wadau zaidi ya 2000 kutoka nchi mbalimbali duniani.
Pamoja na mambo mengine alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha sekta ya madini nchini kupiga hatua na kuwa mfano wa kuigwa kwa nchi za Afrika Mashariki na kusini mwa Jangwa la Sahara.
“Natoa wito kwa wadau wa sekta hii kuendelea kushirikiana na serikali ili kufikia malengo yaliyowekwa na wizara husika hasa ikizingatiwa Tanzania imebarikiwa kuwa na aina mbalimbali ya madini,” amesema.
Alieleza kuvutiwa na sera ya madini ya Tanzania kwa kuwa kiungo muhimu cha maendeleo ya sekta hiyo ya madini, na kuahidi kuishawishi Serikali ya Malawi kuiga sera hiyo.
Aidha, akizungumzia ushindi wa tuzo hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Terry Strong aliishukuru wizara kwa kutambua juhudi za kampuni hiyo katika kutekeleza matakwa ya sheria ya madini kwenye kipengele cha uwajibika wa kampuni kwa jamii.
Pia amesema katika suala la uhifadhi wa mazingira, afya na usalama mahala pa kazi, ni jambo ambalo limepewa kipaumbele na kampuni hiyo katika kujali utu na mazingira endelevu kwa wafanyakazi wake na jamii inayozunguka mgodi huo.