KATIKA jitihada za kuendelea kuboresha sekta ya afya mkoani Geita, Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imetoa msaada wa vifaa tiba kwa Halmashauri ya Wilaya ya Geita na Halmashauri ya Mji wa Geita ikiwa ni mwendelezo wa kudhibitisha dhamira ya kampuni hiyo katika uwajibikaji kwa jamii.
Msaada huo wenye thamani ya Sh260 milioni, unajumuisha vitanda 17 vya hospitali, vitanda vitano vya uchunguzi wa kitabibu, majokofu maalumu ya kukusanya damu na magodoro.
Pia imetoa vifaa maalumu vya uchunguzi wa via vya uzazi kwa mwanamke, viua wadudu, majokofu ya kuhifadhia maiti, vifaa vya upasuaji, mashine za kufulia na darubini.
Akizungumza baada ya kupokea msaada huo jana mkoani Geita, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Kanali Boniphace Maghembe aliishukuru GGML kwa ukarimu wao kwa jamii inayozunguka migodi
“Ni furaha yangu kutambua kuwa tangu GGML ianze kazi hapa Geita, wameshirikiana kwa karibu na Serikali kutekeleza miradi kadhaa ya afya hususan ujenzi wa zahanati na vituo vya afya,” alisema.
Aidha, Meneja Mwandamizi anayesimamia mahusiano endelevu ya kijamii kutoka GGML, Gilbert Mworia, alisisitiza umuhimu wa huduma bora za afya katika kufikia lengo la 3 la Umoja wa Mataifa la Maendeleo Endelevu, ambalo linalenga katika kuhakikisha maisha ya afya na kukuza ustawi kwa wote.
“Lengo la 3 la Maendeleo Endelevu ni miongoni mwa Malengo 17 ya Maendeleo Endelevu yaliyowekwa na Umoja wa Mataifa mwaka 2015, na GGML imejidhatiti katika kuboresha afya na ustawi wa watu,” alisema.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka wa 2000, GGML imejitolea kuboresha ustawi wa jamii inayozunguka mgodi kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa ikiwamo afya, elimu, maji, barabara na miradi ya kiuchumi.
GGML imeboresha upatikanaji wa huduma bora za afya mkoani Geita kupitia mipango mbalimbali, si tu kwa msaada wa vifaa tiba, bali pia kupitia ujenzi wa zahanati na vituo vya afya.