Michuano ya Kombe la Dunia 2018 imeendelea tena leo kwa timu ya taifa ya Denmark kucheza mchezo wake wa pili wa hatua ya makundi dhidi ya timu ya taifa ya Australia.
Mchezo wa Denmark ulikuwa na mvuto zaidi kwa upande wa Tanzania, hii inatokana na uwepo wa staa wa Denmark mwenye asili ya Tanzania Yussuf Yurary Poulsen ambaye mchezo uliopita aliipatia ushindi Denmark dhidi ya Peru wa goli 1-0.
Denmark leo wakicheza mchezo wao wa pili wameambulia sare ya kufungana goli 1-1, goli la Denmark lilipatikana dakika ya 7 kupitia kwa staa wao Christian Eriksen lakini Australia walisawazisha goli hilo dakika ya 38 kwa mkwaju wa penati baada ya Yussuf Poulsen kushika mpira katika eneo la hatari.
Poulsen baada ya kushika katika eneo la hatari na kusababisha penati alioneshwa kadi ya njano ikiwa hiyo ni kadi yake ya pili katika World Cup 2018 na amesababisha penati kwa mara ya pili, Yussuf anakuwa mchezaji wa kwanza katika historia ya World Cup kusababisha penati nyingi (2) katika msimu mmoja toka 1966.
Sare hiyo sasa inawaweka pazuri Denmark kwa kufikisha point nne na wanahitaji point moja tu mchezo ujao dhidi ya Ufaransa ili wafuzu hatua ya 16 bora au kama ikitokea bahati mbaya wakapoteza, basi watahitaji kuomba Peru amfunge Australia mechi ya mwisho huku Ufaransa leo afanikiwe kumfunge Peru.
FULL VIDEO: Zilivyotolewa tuzo za MO Simba Awards 2018