Makamu wa Rais wa Ghana ametangaza kutambulika ramsi kwa Kitambulisho cha Taifa cha nchi hiyo kama hati ya kusafiria kuanzia robo ya pili ya mwaka 2022.
Hatua hiyo ya Ghana inatokana na kutambuliwa kwake kama mwanachama wa Taasisi ya Kimataifa ya Usafiri wa Anga (ICAO), ambapo Kitambulisho kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa kitatumika kama hati ya kielektroniki ya kusafiria.
Zaidi ya nusu ya wakaazi wote nchini Ghana wamepata vitambulisho vya taifa, lengo likiwa kuwasajili wananchi wengi inavyowezekana kufikia mwishoni mwa mwaka 2022.
Taifa hilo la Magharibi mwa Afrika litakuwa moja ya nchi chache duniani zinazotumia kitambulisho cha taifa kama hati ya kusafiria. Kitambulisho cha Taifa nchini humo kinatumika pia kusajili laini ya simu huku serikali ikipanga kutumia kitambulisho hicho kwa shughuli zote za manunuzi ya kidigitali.