Ghasia za magenge nchini Haiti zimewakosesha makazi zaidi ya watoto 300,000 tangu mwezi Machi, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto lilisema Jumanne wakati nchi hiyo ya Caribbean ikipambana kuzuia mauaji na utekaji nyara.
Watoto ni zaidi ya nusu ya karibu watu 580,000 ambao wamekosa makazi katika miezi minne iliyopita. Mgogoro wa ghasia ulianza mwishoni mwa mwezi Februari baada ya mfululizo wa mashambulizi yaliyoratibiwa kwenye miundombinu muhimu ya serikali hatimaye kusababisha Waziri Mkuu Ariel Henry kujiuzulu mwezi Aprili.
“Maafa ya kibinadamu yanayotokea mbele ya macho yetu yanaathiri vibaya watoto,” Catherine Russell, mkurugenzi mtendaji wa UNICEF, alisema katika taarifa. “Watoto waliokimbia makazi yao wanahitaji sana mazingira salama na ya ulinzi, na kuongezeka kwa usaidizi na ufadhili kutoka kwa jumuiya ya kimataifa.”
Magenge sasa yanadhibiti angalau asilimia 80 ya mji mkuu wa Port-au-Prince na barabara kuu zinazoingia na kutoka humo, huku zaidi ya watu 2,500 wakiuawa au kujeruhiwa kote nchini katika miezi mitatu ya kwanza ya mwaka, kulingana na Umoja wa Mataifa.