Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo September 5, 2017 imepokea kielelezo cha maelezo ya Polisi katika kesi ya Meno ya Tembo inayomkabili raia wa China, Yan Feng Glan maarufu kama Malkia wa Pembe za Ndovu na wenzake.
Kupokelewa kwa kielelezo hicho ni baada ya upande wa utetezi kukataa maelezo ya onyo yaliyochukuliwa Polisi dhidi ya mshtakiwa Salvius Matembo.
Uamuzi huo umetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wa Mahakama hiyo, ambaye amesema kielelezo hicho kimepokelewa kwa sababu kitafaa zaidi wakati wa kuandika hukumu.
>>>”Mahakama inapokea maelezo ya onyo yaliyochukuliwa na Polisi kutoka kwa mshtakiwa Matembo kama kielelezo.”
Baada ya kutoa uamuzi huo, Hakimu Shahidi aliahirisha kesi hiyo hadi September 13, 2017 ambapo itaendelea na ushahidi.
Mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ni Philemon Manase ambapo washtakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi kwa kujihusisha na biashara ya Meno ya Tembo yenye thamani ya Tsh. Bilioni 13.
Washtakiwa hao, wanadaiwa kuwa kati ya January 1, 2000 na May 22, 2014 walijihusisha na biashara ya nyara za Serikali.
Waziri Maghembe kuhusu kuuawa kwa aliyefanikisha kukamatwa “malkia wa pembe za ndovu”