Majimbo 10 ya Marekani yameipeleka mahakamani kampuni ya Google, yakiituhumu kuwa na mienendo ya kukandamiza ushindani kwenye sekta ya matangazo ya biashara mtandaoni.
Google pia imeshutumiwa kula njama na kampuni nyingine kubwa ya Facebook ya kutoa ripoti za kupotosha kuhusu mauzo.
Mwendesha mashtaka mkuu wa jimbo la Texas Ken Paxton aliyetangaza mashtaka hayo, amesema Google inatumia nguvu zake kudhibiti gharama za kutangaza mtandaoni, na kupanga bei kwa njia za kujipendelea na kuwakatisha tamaa washindani.
Google ambayo inayo Makao Makuu katika Jimbo la California imesema madai hayo ya mwendesha mashtaka wa Texas hayana mashiko, kwa sababu imesema gharama za kutangaza biashara mtandaoni za kampuni hiyo zimeshuka sana katika muongo uliopita.
Septemba mwaka 2019 mwendesha mashtaka huyo aliongoza mpango unaowashirikisha wenzake kutoka vyama viwili vikubwa vya Marekani katika majimbo 50, kutaka uchunguzi katika mbinu za kibiashara za Google, ambazo walidai zinaazimia kuihodhi sekta nzima.