Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England Man City baada ya kuongoza Ligi kwa wiki kadhaa leo walisafiri kutoka Manchester hadi London katika uwanja wa Chelsea wa Stamford Bridge kucheza game yao ya 16 ya Ligi Kuu England dhidi ya Chelsea ya kocha Maurizio Sarri.
Chelsea wakiwa Stamford Bridge wamefanikiwa kuivunja rekodi ya Man City ya kutopoteza mchezo wowote wa EPL msimu huu kwa kuifunga kwa magoli 2-0, magoli safi yakifungwa na kiungo wa kifaransa N’golo Kante dakika ya 45 na beki wa kibrazil David Luiz aliyefunga goli la pili dakika ya 78.
Huo ndio mchezo wa kwanza kwa Man City kupoteza msimu huu baada ya kucheza michezo 15 na kushinda 13 sare michezo miwili, hivyo kipigo hicho ni wazi kinamuondoa kileleni na kuwapa Liverpool nafasi rasmi ya kuongoza Ligi wakiwa wamewazidi point moja.
Liverpool kabla ya ushindi wa 4-0 dhidi ya Bournemouth walikuwa wapo nafasi ya pili na walivyoshinda game, hivyo wakapanda hadi nafasi ya kwanza kwa muda wakiombea Man City apoteze ili wajihakikishie nafasi hiyo kwa asilimia 100, sasa unaweza kusema Chelsea kuwafunga Man City kumetoa baraka kwa Liverpool kuongoza Ligi wakiwa na point 42 kama mashabiki wa Liverpool walivyokuwa wanaombea.