Msimu wa tatu wa kambi ya madaktari Bingwa wa Mifupa na mishipa ya fahamu kutoka taasisi ya MOI ambao wako katika kambi tiba ya GSM Foundation inayozunguka nchi nzima kuwafanyia upasuaji watoto waliozaliwa na vichwa vikubwa na mgongo wazi imeweka kambi yake Pwani na sasa wapo Tanga.
Mbunge wa Chalinze Ridhiwani kikwete alifika mwenyewe kujionea na kupaza sauti yake kuwasisitizia Watanzania kujitokeza kupata tiba hii ambayo kiukweli ni ya gharama kubwa na madaktari wataalam wa tiba hizo huwa ni wachache sana lakini GSM wamesimamia kila kitu kikawa bure.
Huu ni mkoa wa 10 kwa kambi hii kutembelea, huku ukiwa ni msimu wa tatu wa kambi tiba zenye lengo la kuokoa maisha ya watoto takriban 3500 ambao hupoteza maisha kila mwaka kwa mujibu wa tafiti za MOI za mwaka 2002.
Tafiti zinasema zaidi ya watoto 4000 huzaliwa kila mwaka lakini ni 500 tu huweza kufika kwenye tiba huku changamoto kubwa ikitajwa kuwa ni uchache wa madaktari na ukubwa wa gharama za tiba.
Awamu ya kwanza ya kambi tiba ya GSM ilipita Mwanza, Shinyanga. Singida, Dodoma na Morogoro, ya pili ikapita Mtwara, Songea, Mbeya na Iringa, na sasa ya tatu ndio inapita katika mikoa ya Pwani, Tanga, Kilimanjaro na Mara.