Kiongozi huyo wa mpito wa Guinea ameliambia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York kwamba bara hilo lilikuwa likiteseka kutokana na “mfano wa utawala uliotwikwa juu yetu” na ambao “hauendani na hali halisi ya mambo”.
“Wakati umewadia muache kutusomea na kutufanya kama watoto,” aliongeza.
Doumbouya alichukua madaraka kupitia mapinduzi ya kijeshi mwezi Septemba mwaka 2021, baada ya miaka 11 ya utawala wa kiraia nchini Guinea.
Aidha ameeleza kuwa mfumo wa kidemokrasia wa mataifa ya Magharibi haufanyi kazi katika mataifa ya bara Afrika.
“Sisi Waafrika tumechoka namna ya hawa na wale mnavyotupangia, hatuungi mkono na hatupingi Marekani, hatuungi mkono na hatuwapinga Wachina, hatuungi mkono wala hatiwapingi Wafaransa, hatuungi mkono wala hatuwapingi Warusi, sisi ni Waafrika tu.” alisema kanali Mamady Doumbouya.
Guinea ni miongoni mwa nchi kadhaa za magharibi na kati mwa Afrika ambazo zimeshuhudia mapinduzi katika miaka ya hivi karibuni zikiwemo Mali, Burkina Faso, Niger na Gabon. Mapinduzi hayo yalilaaniwa vikali na Ecowas, Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa.