Wizara ya afya nchini Guinea ya Ikweta, imesema idadi ya waliofariki kutokana na mlipuko wa virusi vya Marburg iliongezeka hadi 12 kufikia siku ya jana.
Kifo cha kwanza kiliripotiwa mnamo Januari 7, katika mkoa wa Kie-Ntem, kabla ya kusambaa hadi jiji la kibiashara la nchi hiyo, Bata.
Virusi vya Marburg ambavyo vina dalili karibia na vile vya Ebola, husababisha kutokwa na damu na kufeli kwa viungo vya ndani vya mwili, na kifo cha hivi punde kiliripotiwa Aprili, 11, kwa mujibu wa wizara ya afya ya Guinea ya Ikweta.
Mwezi Machi mwaka huu, Shirika la afya Dunia, WHO, liliomba nchi hiyo kuripoti matukio yoyote kwa shirika hilo, WHO, ikihofu kuwa kuenea kwa magonjwa ya kuambukizana yanaweza kuchipuka na kuathiri mataifa jirani ya Gabon na Cameroon.
Kwa mujibu wa WHO, kasi ya vifo ni kutoka asilimia 24 hadi asilimia 88, katika milipuko ya hapo awali, huku aina ya kirusi na uthibiti wa maambukizo yakizingatiwa.
Kwa sasa wanasayansi hawajafanikiwa kupata chanjo lakini matibabu yanayowezekana ikiwa ni pamoja na bidhaa za damu, matibabu ya kinga na matibabu ya dawa, pamoja na chanjo za mapema za muathiriwa, zinatathminiwa.
Virusi hivi vinachukua jina kutoka kwa mji wa Ujerumani, Marburg, mahali ambapo iligunduliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1967, katika mahabara ambapo wafanyakazi walikuwa wametangamana na nyani wa kijani aliyekuwa ameambukizwa, aliyesafirishwa kutoka nchini Uganda.