Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na wakimbiza Mwenge wa Uhuru wa mwaka huu (2018) Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuwapongeza kwa kazi nzuri waliyoifanya.
Pamoja na kuwapongeza wakimbiza Mwenge wa Uhuru, Rais Magufuli amewataka Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya zote ambazo zimekutwa na miradi yenye dosari kutekeleza agizo la Waziri Mkuu la kutoa maelezo ndani ya siku 10 na kurekebisha dosari zilizojitokeza.
Aidha, Rais Magufuli ameagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya katika halmashauri 5 ambazo zimefanya udanganyifu kwa miradi iliyotembelewa na mwenge mwaka jana kutoonekana mwaka huu, wajieleze kwa kina kabla ya kuchukuliwa hatua.
“Waziri Mkuu nataka yale maelezo ya kina watoe sasa, kwa nini wanadanganya Mwenge, kwa nini wanamdanganya Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere ambaye ni kiini na mwanzilishi halali wa Mwenge” amesema Rais Magufuli.