MWANANCHI
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro amepiga marufuku unywaji wa pombe kali aina ya Viroba kwa watu wenye umri kati ya miaka 18-30 pamoja na kupiga marufuku uuzaji wa pombe kiholela.
Waraka uliotolewa na Mkuu wa Mkoa huyo umeonyesha kuanzia Desemba 15 Serikali itaendesha oparesheni maalum ya kuwakamata watu wanaolewa pombe muda wa kazi.
Akielezea hilo Mkuu huyo wa Mkoa amesema ulevi uliokithiri umepelekea kupungua kwa nguvu kazi ya kutosha kutokana na vijana wengi kujiingiza katika unywaji wa pombe unaoathiri afya zao.
MWANANCHI
Mtu mmoja amefariki kutokana na tetenasi ambayo ilisababishwa na kidonda alichokipata wakati anabandua kucha za bandia alizobandika wakati siku ya harusi yake.
Mtu huyo Sophia Komba alifunga ndoa Oktoba 15 na Richard Mmary, ambapo mume wake anasema wiki moja baada ya kufungwa ndoa hiyo Sophia alimuaga anaenda saluni kutoa kucha, aliporudi baada ya saa mbili alikuwa analalamika sana kuumwa na kidole ambacho kilipata kidonda kutokana na kubanduliwa kucha vibaya na kuumia.
Mume wake anasema hakujua ukubwa wa tatizo hivyo akamnunulia Spirit na kumpaka, lakini tatizo likaendelea kuwa kubwa na mpaka anafariki daktari alithibitisha kuwa mwanamke huyo amefariki kwa tetenasi.
Wamiliki wa saluni waliohojiwa wamesema kuwa gundi inayofaa kubandikia kucha huuzwa ghali hivyo huenda saluni iliyomhudumia marehemu huyo walitumia gundi ya bei nafuu ambayo siyo salama, huku mtu mwingine anayejishughulisha na kubandika kucha hizo akisema iwapo kucha hizo zinakaa muda mrefu huwa na madhara kwa binadamu.
NIPASHE
Zahanati ya Mtepeche iliyopo Wilayani Nachingwea, Lindi inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mzani wa kupimia watoto baada ya kuzaliwa kwa zaidi ya kipindi cha mwaka mmoja, huku uchunguzi wa gazeti hilo ukibaini kuwa mzani mmoja unagharimu kati ya shilingi 250,000/- na 300,000/-.
Mganga Mfawidhi wa Zahanati hiyo Ibrahimu Mpini amesema changamoto hiyo imefanya wasijue uzito wa watoto wanaozaliwa na jitihada walizozifanya hazijazaa matunda yoyote mpaka sasa Zahanati hiyo kuwa na mzani.
Mbali ya changamoto hiyo, Zahanati hiyo inakabiliwa pia na tatizo la ukosefu wa glovu na pia upungufu wa dawa muhimu ikiwemo Panadol.
JAMBO LEO
Rais wa Malawi Profesa Peter Mutharika ameibuka na kusema kuwa Tanzania haina hata sentimeta moja kwenye Ziwa Nyasa mbele ya Marais Wastaafu Joachim Chissano wa Msumbiji na Festus Mogae wa Botswana walipokutana Malawi.
Rais huyo amesema hayo wakati mgogoro wa mpaka kati ya Malawi na Tanzania ukiwa haujapatiwa ufumbuzi.
“Suala hili liko wazi kabisa kwa mujibu wa Mkataba wa Heligoland wa mwaka 1896 na muafaka wa OAU (sasa Umoja wa Afrika- AU) wa mwaka 1985” alisema Mutharika.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe aliwahi kukaririwa akisema nchi zote husika zinapaswa kuheshimu maagizo ya kuwasilisha ushahidi wa mipaka katika Sekretarieti ya SADC kwa wakati ili wasuluhishi waupitie.
JAMBO LEO
Mkulima na mkazi wa kijiji cha Rosana Wilaya ya Tarime, Matiku Makenge Ghati ameuawa na watu wasiojulikana kwa kukatwa mapanga kichwani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tarime-Rorya, Kamishna Msaidizi Benedict Lazaro Mambosasa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa marehemu kauawa jirani na nyumba yake akiwa anatoka matembezini, mpaka sasa hakuna aliyebainika kuhusika na tukio hilo na upelelezi unaendelea.
Mambosasa alitoa wito kwa jamii kutoa taarifa pale wanapoona vitendo vya kiarifu vinajitokeza ili Jeshi hilo lifike mapema na kuwatia nguvuni watuhumiwa wa tukio husika.
HABARI LEO
Mkazi wa Temeke Leonidas Mathias (42) ambaye ni mwalimu amefikishwa kizimbani katika Mahakama ya Mwanzo Kariakoo kujibu mashtaka ya kumshambulia Askari wa Usalama Barabarani Koplo Machage Novemba 10, Barabara ya Uhuru maeneo ya Clock Tower.
Mathias ameshtakiwa kwa kosa la kumkaba Askari huyo akiwa amevalia sare ya kazi, mshtakiwa amekana kosa hilo na kurudishwa rumande mpaka Desemba 3 ambapo kesi hiyo itatajwa tena.
HABARI LEO
Ofisa Elimu Taaluma Mkoa wa Rukwa, Fanuel Mkaruka amesema wanafunzi 808 wa kike kutoka shule za msingi na Sekondari Rukwa wamekatiza masomo yao baada ya kupata ujauzito katika kipindi cha miaka minne iliyopita, ambapo kati yao 59 ni wanafunzi wa shule ya msingi huku 749 wakiwa wa sekondari.
Zimetajwa baadhi ya sababu kubwa zinazopelekea wanafunzi wengi wa kike kuacha masomo kuwa ni pamoja na mimba na tatizo la fikra iliyojengeka kwa watu wengi kwamba mtoto wa kike ni wa kuolewa tu.
Amezitaja baadhi ya changamoto zinazofanya changamoto hizo kuendelea kuwepo kuwa ni pamoja na wasichana wanaopewa ujauzito kutotoa ushirikiano kwa vyombo vya dola kuwataja wahusika.
Ofisa mradi wa unaofadhiliwa na Sweden TMEP Fausta Valery amesema mradi huo umechangia kupunguza tatizo hilo kwa asilimia 10 pekee.
UHURU
Victor Kanyari ambaye anayeendesha kanisa la Salvation Healing Ministry amegundulika kuwa ni tapeli baada ya kufichuliwa na kipindi cha Tv cha “Inside Story” baada ya kubainika juu ya mchezo anaoufanya na kundi la wafuasi wake ambao hutoa ushuhuda wa uongo kwa kujifanya wamepona.
Jamaa huyo ambaye amekuwa akifanya huduma zake Nairobi Kenya aliweza kujikusanyia imani za watu wengi kwa kuwa amekuwa akilenga masikini ambao walikuwa tayari kutoa kidogo walichonacho ili wapate msaada wa mchungaji huyo.
Baada ya jamaa huyo kugundulika imepelekea Serikali kupiga marufuku usajili wa makanisa mapya, huku kukiwa na agizo la makanisa yote kujisajili, agizo ambalo limeonekana kutozingatiwa.
Moja ya watu waliohojiwa amesema; “.. Kanyari ni Mkenya wa kawaida, mwenye njaa, anayetafuta kula, hadhi na madaraka. Kama mtu aliyekuwa naye darasani hivi sasa ni mbunge na anaweza kumpita akiendesha gari la kifahari atajiuliza ‘Nimewezaje name kuendesha kama hilo’..”