Polisi wa Kenya Jumatano walisema “hakuna maandamano yatakayoruhusiwa” Katikati mwa mji mkuu, Nairobi, kufuatia maandamano ya kuipinga serikali, yaliyosababisha vifo.
Nchi hiyo imekumbwa na maandamano yaliyokuwa ya amani hapo awali ambayo yalichochewa na muswada uliotupiliwa mbali wa kuongeza ushuru, na kugeuka maandamano ya vurugu yaliyosababisha vifo vya watu kadhaa, kulingana na kundi la haki za binadamu linalofadhiliwa na serikali.
Rais William Ruto amekabiliwa na changamoto ya kutuliza hali hiyo, kwa kutosaini muswada wa fedha uliopendekeza kuongezwa kwa ushuru, kulivunja baraza la mawaziri na kuahidi kupunguza matumizi ya serikali.
Lakini maandamano ambayo si makubwa ukilinganisha na mwezi uliopita, yaliendelea nchini kote, huku wengi wakimuomba kiongozi huyo wa Kenya kujiuzulu.