Rais William Ruto amewataka Wakenya kujisajili katika Hazina ya Bima ya Afya ya Kijamii (SHIF). Huu ni mfumo mpya wa bima ya afya, baada ya ule wa awali kufutiliwa mbali.
Katika mpango huo, alisema, watu wa kipato cha chini watachangia hadi shilingi 300 ya Kenya (takribani dola 2.2) kwa mwezi, huku serikali ikiwalipa wale ambao hawawezi.
“Sasa tuna sheria inayoanzisha Mfuko wa Magonjwa Magumu, ambao utatumika kukidhi gharama za magonjwa kama saratani. Hakuna Mkenya atakayelazimika kuuza mali yake ili kulipa bili za matibabu,” Rais Ruto alisema.
Rais alisema serikali ina nia ya dhati ya kuhakikisha kuwa hakuna anayeachwa nyuma wakati wa utekelezaji wa Mpango wa Afya kwa Wote (UHC) ukiendelea.
Kiongozi huyo alisema mkakati huo mpya utahakikisha kwamba hakuna Mkenya anayesukumwa katika umaskini kwa sababu ya gharama kubwa za matibabu.
Mfumo wa bima ya afya ya awali ulikuwa unalenga kuwatoza wale ambao walikuwa na mishahara tu, lakini mpango mpya utahusisha kila mtu.