Waziri mkuu Kassim Majaliwa amesema Mkutano wa Tatu wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kundi la G77 na China umeazimia kwamba nchi hizo pamoja na China zitaendelea kuweka utaratibu wa kuwakutanisha wataalamu wao kupitia wizara mbalimbali hususan katika maeneo ambayo wameyaainisha ili kuhakikisha hakuna nchi itakayoachwa nyuma kwenye mabadiliko ya sasa ya sayansi na teknolojia duniani.
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amesema kikao hiko pia kimezungumzia maendeleo ya nchi wanachama katika nyanja mbalimbali zikiwemo za kisiasa, kiuchumi, kijamii, ulinzi na usalama pamoja na mwenendo wa uwekezaji kwenye mataifa hayo na kuona namna ambavyo wanaweza kujiimarisha wenyewe.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana Januari 22, 2024 wakati alipomwakilisha Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Tatu wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kundi la G77 na China uliofanyika katika ukumbi wa Rwenzori Speke Resort Munyonyo jijini Kampala nchini Uganda. Mkutano huo ulianza Januari 21, 2024 na kuhitimisha Januari 22, 2024.
Akitoa kauli ya Tanzania katika mkutano huo, Waziri Mkuu alisema nchi inaunga mkono mipango yote iliyoratibiwa na wataalamu kutoka nchi zinazounda umoja huo wakiwemo wa kutoka Tanzania kuhakikisha kwamba Taifa linakuwa sehemu ya mafanikio kulingana na mipango iliyopo kwenye nchi hizo zinazounda kundi la G 77 na China.
“Upande wa kisiasa tutaendelea kuimarisha mahusiano yetu ya kidiplomasia ambayo Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuanzishia na anaendelea nayo vizuri kuhakikisha tunaendelea kuwa na mahusiano ya kidiplomasia na nchi mbalimbali. Vilevile kwenye sekta ya uchumi kama ambavyo Taifa letu limeendelea kuimarisha uchumi wa ndani kwa kutumia fursa tulizonazo kwa kushirikisha marafiki wanaoweza kutuletea mitaji.”
Pia, Mheshimiwa Majaliwa alitaja mkakati mwingine uliowekwa na Taifa katika kukuza uchumi ni pamoja na kuimarisha sekta ya kilimo ambayo inashirikisha watu wengi katika jamii.