Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kimesema hakuna vazi maalum la kuvaa katika maandamano yao ya amani yanayotarajiwa kufanyika January 24,2024 jijini Dar es Salaam.
Mbali na hilo pia wamesema hadi sasa wameshapokea barua kutoka kwa Makamanda wa Polisi wa Wilaya juu ya kuwaruhusu kufanya maandamano hayo ambayo pia wataongozwa na Jeshi la Polisi.
Kauli ya CHADEMA inakuja baada ya kuwepo kwa sintofahamu ya kukubaliwa ama kukatiliwa na Jeshi la Polisi kufanya maandamano hayo.
Akizungumza na Ayo Tv, John Mrema ambaye ni Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje amesema hadi wakati huu wameshapokea barua kutoka kwa baadhi ya Makamanda wa mikoa ya Kipolisi ya Wilaya ikiwemo Kariakoo na Buguruni.
“Mpaka jioni hii tumepokea barua kutoka Jeshi la Polisi wakitutaarifu maandamano yetu yatakuwepo na wao watakuwepo kutuongoza na hizi zimeandikwa na Makamanda wa Polisi wa Wilaya ambapo tuliandika barua maandamano yetu yatakapopita,”.
Kuhusu suala la mavazi na maandalizi Mrema amesema”Sisi tunaendelea na maandalizi yetu kabambe na tunawakaribisha wananchi wote wa Dar es Salaam katika maandamano yetu kwa sababu ni maandamano ya wananchi hakuna vazi rasmi kila mtu avae vazi lake ambalo anaona linafaa kwa maandamano tukutane Kituo cha Buguruni na Mbezi asubuhi mapema ili tuanze maandamano yetu ya amani,”.