Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesisitiza haja ya kusitishwa mapigano kwa sababu za kibinadamu na kutumwa misaada zaidi huko Gaza, akisema kuwa hali ya eneo hilo la Palestina linaloshambuliwa na Israel ni “ya kutisha” na “janga”.
Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, alisema jana Jumatano kuwa ndani ya siku chache, maelfu ya watu wa Gaza wameuawa na kuongeza kuwa: Mafuta bado hayaruhusiwi kuingia Gaza na maji “ni machache sana” na kwamba kuna uhaba wa dawa na vifaatiba mahospitalini.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameyataja mashambulizi ya utawala ghasibu wa Israel huko Gaza kuwa ni makosa ya waziwazi na akaongeza: Ninaitaka Israel iheshimu sheria za vita.
Wakati huo huo, Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk ameyataja mauaji makubwa yanayofanywa na Israel dhidi ya raia wa Palestina pamoja na kuwahamisha raia, wanawake na watoto kwa lazima na kinyume cha sheria kuwa ni uhalifu wa kivita.