Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga, tarehe 9 Novemba, 2023 Jijini Dodoma wakati akijibu maswali ya Wabunge waliotaka kufahamu mpango wa Serikali katika kumaliza changamoto za umeme nchini.
Amesema, Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) imeendelea kuimarisha Hali ya Upatikanaji wa Umeme nchini ambapo hadi sasa imefanikiwa kuongeza 125 MW katika Grid ya Taifa kutoka vyanzo vya Gesi asilia na mafuta sambamba na ongezeko la uwezo wa uzalishaji katika vituo vya maji vya Pangani na Kidatu kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Aidha, Naibu Waziri Kapinga ameeleza zaidi kuwa, pamoja na jitihada hizo, Serikali pia imeongeza uzalishaji wa gesi katika visima vya Mnazi Bay, Somanga na Madimba ili kuweza kuongeza gesi ya kuzalisha umeme na kupunguza changamoto ya kukatika kwa umeme katika maeneo mbalimbali nchini.
Vilevile inaendelea na matengenezo ya mitambo ya kuzalisha umeme ili kuboresha zaidi Hali ya Upatikanaji wa Umeme nchini.
Vile vile, ameendelea kuwasisitiza Mameneja wa TANESCO, kuweka utaratibu mzuri wa mgao wa umeme katika Taasisi zinazotoa huduma kwa wananchi ikiwemo Vituo vya Afya, Ofisi za Serikali, Mashule na n.k ili wananchi waendelee kupata huduma.
Akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Christine Ishengoma aliyetaka kufahamu kumalizika kwa tatizo la umeme katika Manispaa ya Morogoro, Mhe. Kapinga, amesema Serikali imefunga mashineumba yenye uwezo wa MVA 120 katika Kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme cha Msamvu ili kutatua changamoto ya kukatika kwa umeme kwa mkoa huo.
Mhe. Kapinga alifafanua kuwa, kazi hiyo ya kufunga mashineumba itagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 10.5 na inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu wa Novemba 2023.