Hamas imesema ilifikia makubaliano ya kukomesha ucheleweshaji wa Israel katika kuwaachilia wafungwa 620 wa Kipalestina ambao walipaswa kuachiliwa wiki iliyopita, baada ya kuunga mkono upande wake wa makubaliano ya kusitisha mapigano kwa kuwaachilia mateka sita wa Israel kutoka Gaza.
Hamas ilithibitisha Jumatano kwamba Israel itawaachilia wanawake na watoto zaidi wa Kipalestina kutoka magereza yake siku ya Alhamisi, wakati kundi hilo litakabidhi kwa wakati mmoja miili ya mateka wanne wa Israel.
Israel ilikuwa imechelewesha kuachiliwa kwa wafungwa 600 wa Kipalestina siku ya Jumamosi ikipinga kile ilichosema ni unyanyasaji wa kikatili wa mateka wa Israel waliokuwa wakikabidhiwa na Hamas. Hamas walisema huu ni ukiukaji mkubwa wa makubaliano hayo.
Sasa inatarajiwa kwamba wafungwa hao wataachiliwa pamoja na kundi jingine, ikiwezekana baadaye Jumatano au Alhamisi, badala ya kurejeshwa kwa miili ya mateka wanne.
Hilo lingefungua njia kwa mjumbe wa Marekani Mashariki ya Kati Steve Witkoff kuzuru eneo hilo. Amesema anataka Israel na Hamas kuanza mazungumzo yaliyocheleweshwa kuhusu hatua ya pili ya usitishaji mapigano.