Afisa mkuu wa Hamas alisema Jumatano kwamba litajibu pendekezo la kusitisha mapigano lililotolewa na Israel “hivi karibuni “, na kusisitiza haja ya kukubaliana juu ya usitishaji vita wa kudumu.
Pendekezo hilo la Israel linajumuisha kusitisha mapigano kwa siku 40 na kubadilishana wafungwa wa Israel wanaoshikiliwa Gaza na Wapalestina wanaozuiliwa katika jela za Israel.
Suhail Al-Hindi aliiambia Agence France-Presse jana kwamba Hamas itatoa majibu yake kwa uwazi ndani ya muda mfupi sana, ingawa hatasema kwa usahihi ni lini hilo lilitarajiwa kutokea. Serikali ya Israel, ambayo iliwasilisha ombi lake la hivi punde kwa Hamas kupitia wapatanishi wa Misri mwishoni mwa wiki iliyopita, ilikuwa ikitarajia jibu kufikia Jumatano jioni, afisa mmoja aliliambia gazeti la Times of Israel.
Chanzo kinachofahamu mazungumzo hayo kilisema kuwa wapatanishi wa Qatar wanatarajia jibu kutoka kwa Hamas ndani ya siku moja au mbili.
Chanzo hicho kilidai kuwa Israel ilifanya “makubaliano” ikiwa ni pamoja na kipindi cha “utulivu wa kudumu” baada ya kusitishwa kwa mapigano na kubadilishana wafungwa.
Mapema Jumatano, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema wakati wa mkutano na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken kwamba matakwa ya Hamas ya kusitisha vita dhidi ya Gaza hayataleta makubaliano ya kubadilishana wafungwa.
Afisa wa Israel aliiambia AFP kwamba serikali “itasubiri majibu hadi Jumatano jioni” kabla ya “kufanya uamuzi” kuhusu kutuma wajumbe Cairo.