Hamas imekataa pendekezo la hivi punde la kusitisha mapigano, ikiishutumu Israel kwa kupuuza matakwa yake ya msingi, ambayo ni pamoja na kumalizika kwa vita na kujiondoa kikamilifu Gaza.
Katika taarifa mwishoni mwa Jumatatu, kundi hilo la wanamgambo lilisema lilikuwa limewafahamisha wapatanishi kwamba linashikilia msimamo wake wa asili, uliowasilishwa mapema Machi.
Ilisema Israel haijajibu madai yake ya msingi ya “kusitishwa kwa mapigano kamili, kujiondoa (Waisraeli) kutoka Ukanda huo, kurejea kwa watu waliokimbia makazi yao na kubadilishana wafungwa halisi.”
Kauli hiyo imekuja muda mfupi baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitisha azimio la kutaka kusitishwa mara moja kwa mapigano na kuachiliwa kwa mateka wote wanaoshikiliwa huko Gaza.
Kura hiyo ilizua mzozo kati ya Israel na Marekani, ambayo iliamua kutotumia mamlaka yake ya kura ya turufu Jumatatu. Kujibu, Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu alighairi ziara iliyopangwa ya wajumbe wa ngazi ya juu huko Washington.