Katika Mdahalo wa kwanza wa Urais Jumanne, Mgombea wa Republican na Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, alimshutumu Makamu wa Rais Kamala Harris kwa kuwa na msimamo wa kupinga Israel alipo toa wito wa kusitishwa kwa vita hivyo vya Israel na Palestina.
Trump alidai kuwa Harris anachukia Israel na akasema kuwa iwapo atakuwa Rais, Israel haitakuwapo ndani ya miaka miwili huku Harris mwenyewe akikanusha jambo hilo.
Aidha Harris alijibu kwa kusema kuwa ameiunga mkono Israel katika maisha yake yote na kazi yake, pia alisisitiza kuwa Israel ina haki ya kujilinda dhidi ya vitisho, ikiwa ni pamoja na kutoka kwa Iran na washirika wake, lakini akaongeza kuwa jinsi Israel inavyofanya hivyo ni muhimu.
Alisema, “Vita hivi lazima vikome mara moja.” Harris pia alielezea wito wa kupatikana kwa makubaliano ya kusitisha mapigano na kurudishwa kwa mateka walioko Gaza. Pia, alirejelea msimamo wake wa kutafuta suluhisho la mataifa mawili katika mzozo wa Israeli na Palestina ambao umesababisha kupoteza maisha ya watu wengi haswa wa Kipalestina ikiwa pamoja na Watoto na Wanawake.
Trump aliongeza kuwa Harris hajakutana na Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu, alipotoa hotuba muhimu, na akaendelea kudai kwamba Sera zake zingeweza kuangamiza sio tu Israel bali pia watu wa Kiarabu na Wayahudi.