Ofisi ya Shirika la Afya Duniani (WHO) barani Afrika tarehe 11 mwezi Novemba ilifanya mkutano na wanahabari mjini Brazzaville nchini Jamhuri ya Congo, ambapo imesema idadi ya watu walioambukizwa virusi vya Corona barani Afrika imezidi milioni 8.5, na watu zaidi ya laki 2.19 kati yao wamefariki.
Kutokana na kiwango kidogo cha upatikanaji wa chanjo za Corona barani Afrika, wagonjwa wa kisukari barani humo wanakabiliwa na tishio kubwa la kufa kama wakiambukizwa virusi vya Corona.
Mtaalamu wa afya ya umma wa ofisi hiyo amesema uchunguzi wa awali uliofanywa kwa nchi 13 za Afrika umeonyesha kuwa kiwango cha vifo vya maambukizi ya Corona kwa watu wenye ugonjwa wa kisukari kinazidi asilimia 10, lakini kiwango cha vifo vya maambukizi ya Corona katika Afrika nzima ni asilimia 2.5 kwa wastani. Hali hiyo imeonyesha umuhimu wa kukabiliana na ugonjwa wa kisukari barani Afrika.